06/05/2023
*DC JOKATE AFANYA ZIARA BANDARI YA TANGA, AMEWATAKA WAFANYABIASHARA KUTUMIA BANDARI HIYO KUSAFIRISHA BIDHAA ZAO.*
Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Mkoani Tanga, Mhe. Jokate Mwegelo amefanya ziara katika Bandari ya Tanga akiwa na Wafanyabiashara, Viongozi wa Chama na Serikali, Wakulima na Wadau wengine wa Korogwe ambapo amesema lengo ni kujionea maboresho ya Bandari hiyo yaliyotumia zaidi ya Tsh. Bilioni 400 na kuwapa chachu Wana Korogwe kusafirisha bidhaa zote Tanga badala ya kutegemea Bandari ya Dar es salaam pekee.
Akiongea na Waandishi wa Habari Bandarini hapo DC Jokate amesema “Uwekezaji mkubwa umefanyika hapa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan zaidi ya Bilioni 400 katika maboresho ya Bandari ya Tanga , mnaona Meli hii kubwa huko nyuma ilikuwa haiwezi kufika, tumekuja Wafanyabiashara na lazima tukubaliane tani tunazozalisha wote tusafirishe hapa”
“Tukubaliane na Wakala wa Meli ili wapunguze tozo zao lakini ili apunguze lazima awe na uhakika wa kuondoa kontena kadhaa, malengo yetu ni kwamba bidhaa zote zinazozalishwa Wilayani Korogwe tutumie Bandari ya Tanga, ili fedha nyingi zilizowekezwa hapa ziwe na tija”
Kwa upande wake Meneja wa Bandari ya Tanga, Masoud Mrisha amesema “Kwa harakaharaka kuanzia January hadi Machi,2023 tumekusanya zaidi ya Tsh Bilioni 7, baada ya uwekezaji wa Bilioni 429.1 maendeleo ni makubwa, kwa mwaka tulikuwa tunazalisha tani Laki 7.5 lakini baada ya maboresho tunazalisha mpaka tani Mil 3, meli kubwa sasa zinaingia moja kwa moja katika bandari yetu ya Tanga”