
09/08/2025
Je, Mungu anatupa mitihani kwa kutupenda au kutujaribu?
Nilikuwa nimekaa kwenye benchi la kivulini, nikitafakari maisha, ghafla mzee mmoja akanikaribia huku akitabasamu kwa uchovu.
Akanikalia pembeni, akasema kwa sauti ya upole:
"Kijana, umewahi kujiuliza kwanini baadhi ya watu wazuri hupitia mateso makubwa kuliko hata wabaya?"
Nikamtazama, nikasema:
Labda ni kwa sababu Mungu anawapenda zaidi, na anawapa majaribu ili kuwatengeneza.
Akatikisa kichwa taratibu, akavuta pumzi ndefu, akasema:
Lakini, k**a kweli anawapenda, kwa nini asiwaondolee hayo maumivu? Je, mapenzi ni lazima yaje na majeraha?
Nikamjibu:
Pengine ni ili tuwe na nguvu zaidi, na tuwe mfano kwa wengine.
Akanicheka kidogo, kisha akaniuliza:
Wewe ulizaliwa ukiomba kuja duniani au uliumbwa bila kuulizwa?
Nikashindwa kumjibu.
Akaendelea:
K**a sikuwahi kuomba kuzaliwa, halafu niwekwe kwenye dunia yenye magumu na dhambi, je, ni haki kunihukumu kwa kushindwa kwenye mitihani niliyoitupa bila kuomba?
Nilihisi maneno yake yanapiga moja kwa moja moyoni.
Nikamuuliza:
Kwa hiyo unamaanisha nini?
Akasema:
Naamini Mungu wa kweli hawezi kuweka roho aliyoiumba kwenye moto wa adhabu kwa kushindwa mtihani ambao hakuuomba kuufanya. Mapenzi ya kweli hayatoi changamoto ili kuona nani ataanguka, bali yanasaidia wote wasianguke.
Nikabaki kimya, nikihisi dunia imeniondokea kidogo, k**a vile alikuwa amenionyesha upande wa ukweli ambao sikuwa nimeuwazia.
Alipoinuka kuondoka, alinigeukia na kusema:
Kumbuka, si kila jaribu ni upendo na si kila maumivu ni adhabu. Wakati mwingine, ni sisi hatuelewi tu mpango mzima.
Nikamwangalia akienda, nikabaki na swali kichwani:
Je, kweli tunajaribiwa au tunapendwa?