24/12/2025
USAJILI WA YANGA MSIMU HUU: NANI WA KULAUMIWA? INJINIA HERSI ATUPE MAJIBU.
Msimu wa mashindano unaoendelea, klabu ya Young Africans SC ilifanya usajili mkubwa wa wachezaji wapya kwa lengo la kuimarisha maeneo mbalimbali ya kikosi ikiwemo kiungo, ulinzi na safu ya ushambuliaji.
Usajili huo uliibua matumaini makubwa miongoni mwa mashabiki, wengi wakiamini Yanga ingeruka kiushindani ndani na nje ya nchi.
Hata hivyo, baada ya michezo kadhaa kupita, tathmini ya uwanjani inaonyesha kuwa kwa zaidi ya asilimia 80, usajili huo haujaleta matokeo yaliyotarajiwa.
Wachezaji wengi wapya wamekuwa na mchango mdogo ndani ya kikosi, hali iliyolazimisha benchi la ufundi kuendelea kuwategemea wachezaji wa zamani kuibeba timu katika nyakati ngumu.
Mpaka sasa, Mohammed Hussein ndiye mchezaji pekee kati ya waliosajiliwa aliyefanikiwa kujihakikishia namba ya kudumu katika kikosi cha kwanza na kuonyesha kiwango kinachokubalika uwanjani.
Kwa upande mwingine, wachezaji k**a Frank Assinki, Lassine Kouma, Musa Konte, Mohammed Doumbia, Andy Boyeli na Celestine Ecua bado hawajaonyesha mchango wa kuridhisha unaolingana na matarajio ya usajili wao.
Licha ya hali hiyo, sauti za ukosoaji zimekuwa chache, jambo linalozua maswali mazito: Je, tatizo ni wachezaji wenyewe, benchi la ufundi, au uongozi uliofanya maamuzi ya usajili? Kiongozi tunayemuita bora, je kweli ameleta kilicho bora kwa maslahi ya klabu?
Kwa kuondoa Tshabalala, ambaye naye ameonyesha dalili za ubora, bado hakuna mchezaji mpya anayetoa kitu cha ziada kinachoweza kuibadilisha timu pale mambo yanapokwenda kombo. Swali linalobaki ni moja—je, mashabiki hawaoni hali hii au tayari wameridhika?
Haya ni maswali yanayohitaji majibu ya wazi, kwa sababu Yanga kubwa haiwezi kujengwa kwa jina la usajili pekee, bali kwa mchango halisi unaoonekana uwanjani.