10/08/2025
KOSA LA JASMINE RAZAK NI LIPI?
Jasmine Razak ni mwanasheria na wakili wa michezo ambaye amejiwekea heshima kubwa kwa kutetea maslahi ya wachezaji anaowasimamia kwa weledi wa hali ya juu katika nyanja za sheria na ushauri wa kitaaluma.
Umaarufu wake ulianza kung’aa wakati alipomsimamia Simon Msuva kwenye mzozo na klabu ya Wydad Casablanca, Morocco. Kupitia juhudi na ujuzi wake, Msuva alishinda kesi hiyo na kulipwa haki zake zote.
Safari ya mafanikio ya Jasmine haikuishia hapo. Alisimamia kwa ustadi uhamisho wa Feisal Salum "Feitoto" kutoka Yanga SC kwenda Azam FC. K**a ilivyokuwa kwa Msuva, Feitoto alihama kwa dau kubwa na kuanza kulipwa mshahara wa heshima. Taarifa za ndani zinaeleza kuwa Yanga alikuwa analipwa milioni 2 tu kwa mwezi, lakini Azam anapata takribani milioni 24 – ongezeko la mara kumi! Hakika, signing fee, mshahara na marupurupu yake vilipanda maradufu chini ya usimamizi wa Jasmine.
Umahiri wake uliendelea kung’aa aliposimamia dili kubwa la Fiston Mayele kutoka Yanga SC kwenda Pyramids FC ya Misri. Licha ya Yanga kumhitaji, Waarabu walikuja na dau nono na kumchukua. Kwa sasa Mayele analipwa mara saba zaidi ya alivyokuwa Yanga, na motisha hiyo imemsaidia kung’ara hadi kufanikisha ubingwa wa CAF Champions League.
Kwa rekodi hii safi ya mafanikio – kutoka kwa Msuva, Feisal, hadi Mayele – ni swali linalozuka: kwa nini kwa Clement Mzize mambo yamekwama?
Mzize ni mchezaji anayehitajika na vilabu vikubwa kutoka Uarabuni na Ulaya. Thamani yake imepanda sana ukilinganisha na mwaka jana. Hata hivyo, Yanga SC wanagoma kumuuza licha ya ofa zenye uwezo wa kulipa dau wanalodai.
Ikiwa Yanga wanamwitaji, basi wanapaswa kumpa mshahara unaoendana na thamani yake. Mshahara wa milioni 15 kwa mwezi si kiwango cha staa wa hadhi ya Mzize. Kwa kipimo cha soko, analingana kulipwa angalau dola 30,000 (takribani milioni 78) kwa mwezi. Ni jambo la kushangaza kuona Prince Dube akimzidi mshahara ilhali mchango na work rate ya Mzize uwanjani ni mkubwa zaidi.