17/08/2025
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameshiriki uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa reli ya kisasa ya kutoka Uvinza hadi Musongati na kuwahahikishia Watanzania na Burundi.
Akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, Majaliwa amesema reli hiyo itakayokuwa na urefu wa km.240 pindi ikikamilika, itakuwa ndiyo reli ya kwanza inayounganisha nchi na nchi katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Katika hafla hiyo iliyofanyika eneo la Musongati, Burundi, Waziri Mkuu amesema kukamilika kwa ujenzi wa reli hiyo kutasaidia kuunganisha masoko na kuendeleza biashara baina ya Tanzania na Burundi.
Kwa upande wake, Rais wa Burundi, Meja Jenerali Evarist Ndayishimiye alisema kuanza kwa ujenzi wa reli hiyo kutatibu shauku ya muda mrefu ya nchi hiyo kuwa na usafiri wa reli.
"Leo ni siku ya furaha sana kwetu. Tumepata jawabu la tangu enzi na enzi. Mwaka 1921, mradi huu ulianzishwa na Wabelgiji kisha wakaja Wajerumani lakini wakashindwa. Leo hii Tanzania na Burundi tumeweza," amesisitiza
Rais Ndayishimiye amempongeza Rais Samia kwa kufikia hatua kubwa za maendeleo. "Ukirudi nyumbani mwambie Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan kwamba tunampongeza sana kwa kuleta maendeleo ya haraka nchini Tanzania."
"Nimekaa Tanzania kwa muda mrefu lakini kwa sasa nikija naweza kupotea. Magomeni napajua, Tabata na Vingunguti napajua, Mwenge napajua, na Kinondoni nilishakaa; lakini kwa sababu ya maendeleo yaliyopatikana, naweza kupotea. Tunamshukuru kwa uongozi wake imara,"
Mapema, Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa ameisema utekelezaji wa mradi huo unaenda sambamba na Ajenda 63 ya Umoja wa Afrika ambayo inataka bara la Afrika liunganishwe kwa mtandao wa reli ya kisasa.