05/08/2026
KAGERA: Wakazi wa Kata ya Kibirizi, Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera, wameiomba Serikali kujenga kituo cha Askari Wanyamapori ili kukabiliana na tatizo la tembo wanaovamia makazi na mashamba yao, hali inayosababisha uharibifu wa mazao na kuhatarisha usalama wa wananchi.
Ombi hilo limetolewa katika mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Ashatu Kijaji, ambae kiserikali ni mlezi wa mkoa wa Kagera ambapo wananchi wamesema uvamizi wa tembo umedumu kwa muda mrefu na umeendelea kuathiri maisha yao pamoja na shughuli za uzalishaji.
Baadhi ya wananchi, akiwemo Anesius Aloyce na Scolastika Deogratias, wameiomba Serikali kuharakisha utekelezaji wa hatua za kudhibiti tembo hao ili kulinda maisha ya wananchi, mazao na mali zao dhidi ya uvamizi unaojitokeza mara kwa mara.
Akijibu hoja hizo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Ashatu Kijaji, amesema Serikali imepanga kujenga kituo cha askari wanyamapori katika eneo hilo ili kuimarisha ulinzi na kuongeza kasi ya kukabiliana na changamoto ya tembo wanaovamia makazi ya wananchi.
Ameongeza kuwa Serikali itaendelea na utaratibu wa kuwaswaga tembo kurejea katika maeneo yao ya hifadhi, huku ikisisitiza ushirikiano kati ya wananchi na mamlaka husika ili kupunguza migongano kati ya binadamu na wanyamapori.
✍🏿 Enock Yoronimo- Bukoba, Kagera
Mhariri: