17/09/2025
âïž| Mkoa wa Njombe Wafanya Tathmini ya Utekelezaji wa PJTâMMMAM
Leo, Septemba 17, 2025, mkoa wa Njombe umefanya kikao cha tathmini ya utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJTâMMMAM), ambayo inatekelezwa katika mikoa mbalimbali nchini, ikiwemo Njombe.
Programu hii inalenga kuhakikisha watoto wanapata malezi bora, lishe ya kutosha, na nafasi ya kustawi kwa njia endelevu.
Kikao hicho kimeongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Mhe. Juma Sweda, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Antony Mtaka, na kilihusisha wadau mbalimbali wakiwemo mashirika binafsi, viongozi wa kidini, vyombo vya ulinzi, maafisa lishe, na wataalamu wa afya na ustawi wa jamii.
Lengo kuu la vikao hivi ni kujenga ushirikiano wa pamoja kati ya sekta mbalimbali, wadau, na taasisi, ili kushughulikia changamoto zinazokabili watoto chini ya miaka 8 kwa njia endelevu na yenye matokeo chanya.
Mambo yaliyoangaziwa katika kikao hiki ni pamoja na:
Kupima mafanikio yaliyofikiwa katika malezi, makuzi, na maendeleo ya awali ya mtoto.
·Kutambua changamoto zilizopo na kuandaa mikakati ya pamoja ili kuboresha utekelezaji.
· Kuimarisha mshikamano kati ya Serikali, jamii, na wadau wengine ili kuongeza kasi ya utekelezaji.
Mkuu wa Wilaya, Mhe. Juma Sweda, ameagiza halmashauri zote kutenga bajeti kwa ajili ya utekelezaji wa afua mbalimbali kwenye maeneo yao, ikiwa ni pamoja na suala la lishe, pamoja na mikakati madhubuti ya kulea watoto kwa ustawi wao.
Shirika la Uwodo, linalotekeleza mradi wa âMtoto Kwanzaâ katika Mkoa wa Njombe, kupitia kwa mkurugenzi wake Hamisi Kasapa limehimiza wazazi kutenga muda wa kuzungumza na watoto wao pindi wanapokuwa nyumbani, ili kujua maendeleo yao katika afya, lishe, elimu, na malezi jumuishi.
Afisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa wa Njombe, Bi. Subilaga Mwaigisya, pia amesisitiza umuhimu wa vituo vya kulelea watoto kutengeneza mazingira rafiki kwa ajili ya watoto kucheza na kujifunza, ili kusaidia ukuaji wa ubongo wa mtoto na kuendeleza uwezo wao wa kijifunza.