25/11/2014
HADITHI: SISI NI WATOTO WA EVA YULE HOUSE GIRL WA ZAMANI
MTUNZI: AMON TAMILWAI.
Vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na stori za vijiweni na mitaani zote zimepambwa na kisa hiki cha dada wa kazi (house girl) aliemsulubisha mtoto mdogo asie na hatia ambaye aliachiwa kumlea. Wazazi, walezi na wananchi wa Afrika mashariki kwa ujumla wameonyesha hisia zao kwa namna mbalimbali na wengi wakilaani ukafiri huu alioufanya dada huyo aliejulikana kwa jina moja tu la VICKY. Watu wengi wamelaani kitendo hicho na kila mtu ametoa maono yake kwamba k**a ingemtokea yeye angemfanya nini VICKY.. Wengi wameguswa na tukio hili na wengi wamemhukumu dada huyu kwa hukumu kuu wengine wakisema anyongwe, afungwe maisha, apigwe mawe mpaka kifo na kadhalika. Adhabu zote zimekuja kutokana na unyama alioufanya kwa mtoto mdogo asiye na hatia. Hakuna hata mmoja kati ya niliowasikia alietamani kumpa dada huyu nafasi ya pili ya kujitetea au kueleza kwa nini ametekeleza unyama huu kwa malaika yule mtoto.
Wakati yote hayo yakiendelea majumbani hali imebadilika, wazazi wameanza kuwa waangalifu na watoto wao ,kila wanapowaacha,wengine wameamua kuwa wanawahi kurudi toka mishughulikoni na wengine wametoa maonyo mbalimbali kwa wadada wa kazi huku wakiwaonyesha mfano wa alichofanya na alichofanyiwa mwenzi wao. Kila dada wa kazi kwa sasa anajitahidi kutimiza wajibu wake na kuonyesha upendo kwa watoto anao walea ili tu kupinga kile alichokifanya mwenzi wao na pia kujijengea kuaminika kwa tajiri wake.
Masikini dada VICKY njia aliyoitumia kufikisha ujumbe kwa DUNIA haikuwa sahihi; hata mimi mdogo wake sijaiunga mkono, sikutegemea k**a angefanya kwa ukatili kiasi kile. Hata k**a alikua na uchungu na hasira zipitazo hasira za mtoa roho, hakutakiwa kufanya unyama ule kwa mtoto. Hakuna mtu atakae muelewa hata akifumbua kinywa chake kueleza kwa nini amefanya vile. Nafahamu hakuna atakae ona uzito wa sababu yake kwa kua amefanya unyama ule kwa mtoto asie na hatia. Na naamini ni mimi tu ndio naweza kuuambia ulimwengu kwa nini Vicky amefanya vile alivyofanya. Labda ulimwengu unaweza kufungua masikio na kusikia hata kwa sehemu sababu iliyompelekea Vicky kufanya vile.
Mimi naitwa VICTA pacha wake na VICKY yule dada wa kazi alie ICU (chumba cha wagonjwa mahututi). Desember mwaka huu mimi na pacha wangu tunatimiza miaka kumi na mi tatu ya umri, lakini maisha yametufundisha kuishi k**a watu wenye umri wa miaka arobaini. Dunia imefumba macho juu yetu tangu siku ya kwanza ya mimba yetu kutungwa. Sitashangaa kumuona dada yangu VICKY akifungwa maisha au akiuwawa kwa sababu tulishakufa siku nyingi ilihali tu hai. Na amini imebaki siku tu mizoga yetu kuliwa na mbwa na hayawani wa Dunia. Sio kuwa tumekata tamaa ya maisha la hasha ila tangu siku ya kuzaliwa kwetu mawingu meusi yalishatanda juu ya anga k**a ishara ya anga na ardhi kutukataa. Jua lilifunguliwa mpaka mwisho na kuelekezwa vichwani mwetu tangu siku ile mbegu za uzazi wetu zilipotungwa, anga halikutamani tupate kimvuli hata siku moja ya uhai. Jasho na fukuto vimetufuata , vilio huzuni, bahati mbaya, uchungu na kila aina ya dhiki hilo ndio limekuwa fungu la maisha yetu kwa miaka yote kumi na mitatu.Ngoja niache nahau na mashairi nianze kuwaeleza kwa ufupi historia yetu.
******************************************************************************
Sisi ni watoto wa pekee wa dada mmoja aliejulikana kwa jina la EVA, najua wengi mme msahau kwa kuwa ni miaka mingi imepita tangu jina lake lifutike katika DUNIA. Usiulize baba yetu ni nani kwa kuwa jibu ndio nitakupatia.
Tulipotimiza umri wa miaka takribani mitatu au minne tangu kuzaliwa mama yetu alituchukua huku akiwa kwenye hali mbaya sana kia afya na kutupeleka kwenye nyumba moja ya kifahari kidogo. Tulipofika getini mlinzi alituzuia lakini mama alimsihi sana amuite mama mwenye nyumba. Yule mlinzi aliita kwa woga kidogo, “mama, mama kuna wageni wako”. Sauti ya mama asiye wa makamo sana ilisikika ikimuamuru mlinzi aturuhusu kuingia. Mama yetu mpenzi alitususuma lakini tulipoingiza nyuso zetu tu getini, yule mama alimaka kwa sauti, “haaaaaa!!!! Haaaaaa!!!haaaaa!!! Eva? Umerudi tena? umefuata nini hapa?”. Sote tulistushwa na sauti ile kali na tulimshika mama yetu aliekuwa anakohoa ili aweze kujieleza. Sitasahau siku ile maishani mwangu, mama yule alikuja na kutusukuma huku akisema, “unataka nini? Umekuja kunichafulia familia yangu tena eeee??” mama kwa kujikongoja alianza kuongea na maneno yake nayakumbuka mpaka leo. “Mama mimi sijakuja kwa shari, naomba unisikilize kidogo tu kisha nitaondoka,|” yule mama akiwa anajifunga kibwebwe chake vizuri alitema mate kwa dharau kisha akasema eehhh ongea…. Mama aliendelea, “Dada mimi nitakufa siku si nyingi, nimejitahidi sana kuwalea hawa watoto tangu siku ya kwanza ya ujauzito mpaka leo, nimefanya kila niwezalo kunusuru uhai wao, lakini mpaka sasa hali yangu si njema tena. naumia sana kwamba nitawaacha hawa watoto wakiwa hawana msaada wowote; dada naongea maneno haya kutoka moyoni mwangu na wewe ni binadamu tena mwanamke mwenzangu. Naomba unielewe, haki ya mungu dada na apa mbele yako, hawa watoto ni damu yenu. Katika maisha yangu yote ya kukaa hapa kwako k**a house girl sikuwahi kutembea na mwanaume yeyote narudia tena yeyote nje ya wanaume walio humu ndani ya nyumba yako. Najua ukweli unauma ila bora niseme ili kunusuru maisha ya malaika hawa wasio na hatia. Dada, hawa watoto baba yao k**a sio mumeo basi ni watoto wa mwanao mkubwa frank kwa kuwa wote nilitembea nao kwa nyakati tofauti.”
******************************************************************************
Paaaaaaaaahhhh!!!! Sauti kubwa ya kishindo cha kofi kikifuatiwa na yowe kubwa kutoka kwa mama vilitustua na mimi na VICKY tulikimbia moja kwa moja na kumkumbatia mama alierushwa takribani hatua tatu kwa uzito wa kofi lile alilopigwa na yule mama. Tulikuwa wadogo sana lakini uchungu alioupata mama ulitufikia mpaka ndani kabisa na kupasua maini. Mama alizimia pale chini akituacha sisi tukimkumbatia bila msaada wowote. Yule mlinzi alikuja na kumwagia maji na alipo zinduka ali amriwa atuondoe haraka. Alitubeba mzega mzega mpaka nje kisha akafunga geti kwa nguvu pwaaaaaah.
Hapo ndipo nilipojua kuwa sisi tumekataliwa na hatuna namna tena ya kuhesabu kuwa tuna baba. Kwanza hajulikani ni nani kati ya mtoto au baba wa ile nyumba, pili haitatokea yeyote kati yao kuja kutufuata kwa kuwa sisi ni aibu na chanzo cha vurugu katika ile familia. Masikini mama yetu mpenzi, hakuwa na nguvu tena na kutokana na magonjwa yaliyokuwa yakimuandama aliaga dunia na kuacha ulimwengu utulee. Mimi ndio nilikuwa baba wa vicky na vicky alikua mama yangu. Jua, mvua, mitaro, magunia, vyakula vya majalalani na kulala mitaroni ndio yalikua malezi yetu kwa miaka na miaka. K**a binadamu wengine wenye hisia nasi tulihisi uchungu wa Dunia huku tukijua fika tumezaliwa kwa bahati mbaya na ni haramu k**a kilivyo kitimoto kwa muislamu. Hakuna mtu alikuja kutuambia chochote cha kutupa tumaini la maisha zaidi ya kunyanyasika kusiko na mwisho. Wakati watoto wengine wanalelewa kwa upendo na furaha, sisi dunia ilitulea kwa kisirani na chuki, wengine wakiambiwa kuna MUNGU sisi tulijua kuwa MUNGU amefumba macho na masikio tena yuko bize hatuoni. Wakati nyie mnawalisha watoto maneno ya upendo na matumaini sisi Dunia imetulisha chuki, visasi, ugomvi, maonevu na ukatili. Vicky alibakwa akiwa na miaka saba, alianza kufanya kazi za ndani akiwa na miaka tisa ama kumi hivi na kila siku aliniambia kuwa lazima unyama aliofanyiwa mama yetu pamoja na sisi lazima alipe kisasi. Yuko radhi kufa lakini lazima awafundishe walimwengu kuwa binadamu wote ni sawa na tofauti yetu ni mazingira tu.
Sikutegemea k**a atalipiza kisasi kwa mtoto wa Frank ambae anaweza kuwa ndio baba yetu k**a mama alivyosema, lakini pia sidhani k**a frank anamfahamu vicky kuwa ni mmoja wa watoto wa yule house girl aliemuingilia kipindi kile anakaa pale kwao. Ulimwengu haufahamu sababu ya vicky kufanya unyama alioufanya .Vicky atafikishwa mahakani na kush*takiwa na hata hukumu kali itamuangukia. Sina jinsi ya kumsaidia dada yangu mpenzi, moyo wangu umetandwa na huzuni kubwa isiyo mfano. Mikono yangu haina nguvu ya kutengua hukumu yoyote anayopewa wala ile atakayopewa Vicky. Ila asomaye na afahamu liwalo na liwe waambieni wajue SISI NI WATOTO WA EVA YULE HOUSE GIRL WA ZAMANI.
N.B hii ni hadithi ya kubuni tu na majina yalyotumika hayana uhusiano wala ukweli wowote juu ya tukio lolote lililotekea. (KILA JAMBO LITOKEALO CHINI YA JUA LINA CHANZO, SABABU NA MWISHO).