02/04/2026
Aprili 2 na Kifo cha Papa John Paul II.
Tarehe 2 Aprili 2005, dunia ilisimama kwa mshangao na huzuni baada ya kifo cha kiongozi mkubwa wa Kanisa Katoliki, Papa John Paul II. Alifariki akiwa na umri wa miaka 84 katika makazi yake ya Vatican City, baada ya kuugua kwa muda mrefu hasa ugonjwa wa Parkinson's disease.
Alikuwa ni Papa wa kwanza kusafiri sana duniani tofauti na mapapa waliomtangulia, alisafiri zaidi ya nchi 100, akihubiri amani, upendo, na mshik**ano. Alikuwa k**a “raia wa dunia” kuliko kiongozi wa kukaa Vatican City pekee.
Alivunja historia kwa kuingia katika maeneo matakatifu ya dini nyingine. Mwaka 2001, aliingia msikitini huko Damascus jambo ambalo halijawahi kufanywa na Papa kabla yake. Kitendo hiki kilionyesha moyo wa umoja wa dini.
Anakumbukwa kwa kumsamehe mtu aliyetaka kumuua. Mwaka 1981 alishambuliwa kwa risasi na Mehmet Ali Ağca. Kilichoshangaza dunia ni kwamba baadaye alimtembelea gerezani na kumsamehe ana kwa ana, hili lilikuwa somo kubwa la msamaha wa kweli.
Kabla ya kuwa Papa, aliitwa Karol Wojtyła, aliandika vitabu na mashairi, na alikuwa msomi wa Falsafa. Hii ilimfanya kuwa Papa mwenye upeo mpana wa fikra. Hata alipokuwa dhaifu sana kutokana na Parkinson's disease, aliendelea kuonekana hadharani, akionyesha uvumilivu na imani thabiti hadi pumzi yake ya mwisho.
Kifo chake hakikuwa tu mwisho wa maisha ya kiongozi wa dini, bali kilikuwa mwisho wa enzi ya mtu aliyebadilisha historia ya dunia kwa upendo, msamaha, na ujasiri.