18/12/2025
Wagonjwa watano wenye mishipa ya damu iliyoziba kwa asilimia zaidi ya 75 wamefanyiwa upasuaji wa kupandikiza mishipa ya damu ya moyo bila kusimamisha moyo (off – Pump CABG).
Upasuaji huo unafanyika katika kambi maalumu ya siku tano iliyoanza Desemba 16, 2025 na kufanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Hospitali ya Jaslok iliyopo Mumbai nchini India.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya amesema kambi hiyo ni maalumu kwa wagonjwa ambao mishipa yao ya moyo imeziba hivyo kusababisha ufanyaji kazi wa mioyo yao kuwa chini ya asilimia 35.
“Wagonjwa tunaowafanyia upasuaji katika kambi hii mara nyingi utuchukua ugumu kidogo kuwafanyia upasuaji kutokana na ufanyaji kazi wa mioyo yao, hivyo ili waweze kuwa na matokeo mazuri mara nyingi wenzetu wanafanya upasuaji huu bila ya kuusimamisha moyo k**a ambavyo tunaenda kufanya katika kambi hii”, alisema Dkt. Angela
Dkt. Angela amesema kupitia kambi hiyo wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) watajengewa uwezo ambao utasaidia kutoa huduma kwa ufanisi zaidi kwa wagonjwa ambao mioyo yao imechoka kutokana na kuziba kwa mishipa ya damu kwa asilimia zaidi ya 75.
Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu kutoka Hospitali ya Jaslok iliyopo Mumbai nchini India, Upendra Bhalerao amesema kuwa ameona aungane na wataalamu wa JKCI kuwasaidia wagonjwa ambao kutokana na matatizo ya mishipa ya damu kuziba kwa asilimia zaidi ya 75 wanashindwa kujishughulisha na wakati mwingine hupoteza maisha.
“Wagonjwa tutakaowafanyia upasuaji kupitia kambi hii wataweza kufanya shughuli ndogondogo ambazo hapo awali walikuwa hawezi kuzifanya”, amesema Dkt. Bhalerao
Dkt. Bhalerao amesema kupitia kambi hiyo wataalamu watatoa huduma sambamba na kupata mafunzo yatakayosaidia kupunguza idadi ya vifo vinavyotokana na matatizo ya mishipa ya damu ya moyo kuziba.