17/12/2025
WIZARA YA FEDHA YAITA WADAU KUTOA MAONI YA KUBORESHA MWONGOZO WA USIMAMIZI WA MALI ZA SERIKALI
Wizara ya Fedha imetoa rai kwa wadau kutoa maoni yatakayowezesha kuboresha Rasimu ya Mwongozo wa Usimamizi wa Mali za Umma wa mwaka 2025 utakaosaidia kusimamia mali zilizo kwenye Taasisi za Umma kwa tija na ufanisi zaidi ili kuimarisha na kuboresha huduma zinazotolewa na Serikali kupitia mali hizo.
Rai hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Mali za Serikali, Wizara ya Fedha, Chotto Sendo, wakati akifungua kikao kazi cha kukusanya maoni ya wadau kutoka taasisi 25 za Umma zinazowakilisha Mkoa wa Dodoma, Wasimamizi wa Mali wa Mikoa kutoka mikoa saba (7), Wasimamizi wa Mali za Serikali kutoka Ofisi ya Makao Makuu na Mkoa wa Dodoma, kuhusu Rasimu ya Mwongozo wa Usimamizi wa Mali za Umma wa mwaka 2025, kilichofanyika katika ukumbi wa Kilimanjaro, Treasury Square, Jijini Dodoma.
Sendo alisema, Rasimu ya Mwongozo wa Usimamizi wa Mali za Umma wa mwaka 2025, ambao wadau wanatarajiwa kutoa maoni ya kuuboresha inatokana na fursa mbalimbali zilizojitokeza katika usimamizi wa mali za umma katika kipindi cha utekelezaji wa Mwongozo wa Usimamizi wa Mali za Umma wa mwaka 2019.
Aliongeza kuwa rasimu hiyo pia imejumuisha usimamizi wa mali chini ya ushirikiano wa umma na binafsi (PPP-Projects), Upatikanaji wa mali, matumizi ya mali, usimamizi wa mali za miradi, kushughulikia ajali na potevu za mali za Umma, Ufutaji na uondoshaji wa mali chakavu pamoja usajili wa vyombo vya moto.
Alisema kuwa mwongozo huo utakapokamilika na kusainiwa na Mlipaji Mkuu wa Serikali (PMG) utaanza kutumika pamoja na Kanuni za Usimamizi wa Mali za Umma za mwaka 2024 hivyo kuwataka kujadili kwa uwazi ili kujenga uelewa wa pamoja katika suala la usimamizi wa mali za umma na kuhakikisha utendaji bora ,uwajibikaji wa kifedha na utoaji wa huduma bora.