22/11/2025
Mudir Markaz Kuu wa Taasisi ya Ansaar Muslim Youth Centre (AMYC), Sheikh Salim Barahiyan, amepongeza Chuo cha Ualimu Arafah kwa kuzalisha walimu mahiri na wenye nidhamu, na kukifanya kuwa miongoni mwa vyuo vya kuigwa nchini. Akizungumza leo Novemba 22, kwenye mahafali ya wahitimu wa mwaka 2025, Sheikh Barahiyan amesema chuo hicho kimeendelea kuipa heshima AMYC kutokana na walimu wake kuonesha uwezo mkubwa katika ufundishaji na maadili ya kazi.
Amefafanua kuwa mara kwa mara amekuwa akipokea pongezi kutoka maeneo mbalimbali, ikiwemo idara za serikali. Miongoni mwa pongezi hizo ni kutoka kwa Msimamizi wa Elimu Kanda ya Kaskazini, ambaye amesema umahiri wa walimu wanaozalishwa na chuo hicho umeendelea kurahisisha kazi kwa watendaji wa elimu kutokana na nidhamu yao pamoja na kiwango cha juu cha taaluma wanachokionesha.
Katika salamu zake kwa wahitimu, Sheikh Barahiyan amewahimiza kuongeza elimu ili waendane na mabadiliko ya sifa za ajira, akieleza kuwa ajira nyingi katika sekta ya elimu, hususan mashuleni, sasa zinahitaji kiwango cha kuanzia Diploma.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo hicho, Mwl. Salim Mohamed Salim, amesema uongozi wa kitaaluma utaendelea kuimarisha utoaji wa elimu na kuhakikisha chuo kinaendelea kuwa ngazi muhimu ya kuzalisha walimu wanaoendana na mahitaji ya sasa. Amesema kwa kuwa sehemu kubwa ya jamii imechelewa kupata elimu, chuo kimejipanga kuongeza nguvu katika vitengo vya kitaaluma ili kuhakikisha kila mhitimu anakuwa tayari kushindana katika soko la ajira la ndani na nje ya nchi.
.1