29/11/2025
Kufunguka kwa fursa za kiuchumi mkoani Tanga kumepelekea Shirika la nyumba la Taifa (NHC) mkoani Tanga kujenga jengo la kisasa litakalokuwa na ghorofa 7 katika maeneo ya Mkwakwani jijini Tanga ambapo ujenzi wake utagharimu shilingi bilioni 8.4.
Furza hizo za kiuchumi ni pamoja na Bomba la mafuta, maboresho ya Bandari ya Tanga, kufunguliwa kwa viwanda pamoja na zao la Mkonge zimepelekea mkoa wa Tanga kumiminika wageni kutoka ndani na nje ya nchi ambao wanauhitaji wa makazi na ofisi.
Kufuatia hali hiyo Shirika la nyumba la Taifa (NHC) mkoani Tanga likaanza rasmi ujenzi wa mradi huo na linatarajia kujenga na miradi mengine mikubwa ili kukidhi matakwa ya ongezeko la wateja wanaohitaji nyumba za kuishi pamoja na ofisi.
Akizungumza na Radio nuur fm ofisini kwake leo Novemba 28,2025 Meneja wa Shirika la nyumba la Taifa (NHC) mkoa wa Tanga Mhandisi M***a Patrick Kamendu amesema jengo hilo lipo maeneo ya Mkwakwani na ndio maana likapewa jina la Mkwakwani Plaza.
"Jengo hili litakuwa na ghorofa saba, sakafu ya chini na sakafu ya pili itakuwa ni kwa ajili ya shughuli za biashara, sakafu ya tatu mpaka sakafu ya saba itakuwa ni nyumba za makazi, kutakuwa na nyumba mbili zenye vyumba viwili na nyumba mbili zenye vyumba vitatu kwa kila sakafu" Amesema Mhandisi M***a
Mhandisi M***a amewaasa wananchi kujitokeza kununua nyumba na kupangisha kwani wakati jengo linaendelea kujengwa tayari kuna watanzania wamejitokeza kununua na kupangisha katika jengo hilo.
Kwa upande wake Msimamizi msaidizi wa ujenzi huo Mhandisi John Joseph Mchechu amesema mradi huo upo katika asilimia 16 ambao utekelezaji wake ulianza mwezi June mwaka 2025 na unatarajia kukamilika mwezi June mwaka 2027.
"Nawaasa wananchi wauone mradi huu kuwa ni wao ni mradi ambao upo kwa ajili yao, kuna vyumba vya maduka, kuna nyumba za kuishi na pia kuna ofisi" Amesema Mhandisi John
Na Salimu Omari Ally