25/07/2025
Nyota ya Afrika.
TAYE TAIWO,KISIKI,KIBOKO YA MAWINGA.
Na
Honorius Mpangala
Ukitazama 'lineup' ya Super eagles timu ya taifa ya Nigeria au kikosi cha Olympiaue de Marseille lazima uwaze. Si unajua vikosi vikiwa katika mstari wa kutaka kuingia uwanjani watu hupenda kutazamana k**a nani kaanza kwa timu pinzani. K**a ni winga utaanza kunyanyua shingo yako ili upate kuona alikosimama huyu jamaa. Nywele zake timu timu ,zisizo onyesha dalili ya kukutana na chanuo kwa muda mrefu sana. Zimevurugika mithiri ya nywele za mgonjwa wa akili.
Sura ngumu yenye alama ndogo ndogo ya mipasuko ya mejeraha ya chini ya macho na juu ya macho. Unaweza kuwaza kuwa jamaa alikuwa na kazi ya kubiringisha magogo ya kupasua mbao huko mapori ya misitu ya Goboni au misitu ya pori la Akiba la Moyowosi Kakonko huko Kigoma,au Sao Hill huko Mafinga.
Rangi yake nyeusi yenye kutambulisha uafrika wake asili. Mtu fulani mwenye kimo cha wastani akiwa na urefu Wa sentimeta 183 ni k**a futi 6 hivi. Mjuvi Wa kazi ,mwili uliojengeka kwa misuli iliyojipanga vyema kila sehemu ya mwili wake.
Ni Taye Ismaila Taiwo mchezaji Wa soka. Raia Wa Nigeria aliyezaliwa April 16,1985 jijini Lagos.
Alianza safari ya soka katika klabu ya Gabros nchini Nigeria mwaka 2003 baadae akatua Lobi stars ya hapohapo Nigeria mwaka 2004. Baada ya kufanya vizuri katika timu ya vijana akaonwa na Marseille ya Ufaransa na mwaka 2005 wakamsajili.
Katika klabu ya Marseille ndipo dunia ilimtambua fullback huyu Wa kushoto.Akiwa na uwezo mkubwa Wa kupiga mipira ya faulo kwa kuachia makombora makali. Ni k**a alikuwa anaiga mambo Mengi ya Roberto Carlos.
Wajihi wake Wa kikuda asiyecheka uwanjani,kwake ilikuwa kazi kazi hadi dakika ya tisini.
Alitua klabu ya Ac Milan 2011 baada ya kuitumikia Marseille kwa muda mrefu. Alipelekwa kwa mkopo katika klabu ya QPR ya uingereza na Dynamo kiev ya Ukraine.
Ac Milan ilimwachia mwaka 2013 alipojiunga na miamba ya Uturuki ya Bursaspor. Alidumu hapo hadi 2015.Alijunga na Klabu ya HJK Helsinki pale nchini Finland na kudumu kwa mwaka mmoja hadi 2016.
Atua Lausanne mwaka 2017 na baadae kubadili upepo mwaka huo huo. Akajiunga na klabu ya AFC Eskilstuna.
AKIPIGA NA ULIMWENGU,AMKARIBISHA NDEMLA.
Akiwa katika klabu ya AFC Eskilstuna nchini Sweden hapo alikipiga na Ulimwengu aliyekuwa katika klabu hiyo. Saidi Ndemla aliwahi pata kwenda kufanya majaribio katika klabu hiyo ikiwa imeshuka daraja toka ligi kuu.Iliposhuka ndipo Taye alipoondoka na kwenda kujiunga na klabu ya Rovaniemen Palloseura mwaka 2018 inayo julikana k**a RoPs anakocheza hadi sasa.
AITUMIKIA SUPER EAGLES MIAKA NANE.
Tangu mwaka 2004 akiwa Olympique Marseille aliitumikia timu ya taifa ya Nigeria hadi 2012.
Moha vivutio vikubwa toka kwa Taye ni namna alivyokuwa na uwiano mzuri Wa kushambulia na kukaba. Mawinga aliwakomesha kwa tackling murua na ustadi mkubwa Wa kukab kwa akili. Hakika hakuna aliyetaka kukutana na Taye.
BINGWA WA LUPINYO/CHIKWINDA
Wachezaji wengi wana uvaaji Fulani Wa jezi ambao unajenga au kuota mizizi kwao. Kwa hapa Tanzania miaka ya nyuma kidogo Kiungo Wa Simba Hussein Marsha alifahamika kwa namna alivyopenda kuchomekea safi jezi na kuwa msafi nyakati zote.
Sasa Taye alipenda kuchomekea lakini 'bukta' yake aliviringisha kwa kuipindua kiuno chake. Akichomekea halafu anapiga mtindo huo mbao hata Frank Lampard aliuhusudu sana Wa kukunja seheme ya kiunoni 'bukta' yake. Mtindo ule ukiwa Nyasa tunaita Chikwinda au ukiwa Mbeya wanaita Lupinyo.
'Bukta' ikipigwa chikwinda au Lupinyo na winga au Fullback ujue kazi ni pevu. Hata k**a ni kiungo atafanya hivyo ujue kazi ni kubwa katika huo mchezo. Au mwingine huwa ndiyo kawaida yake lazima apige lupinyo au chikwinda ndipo soka lichezwe.
Walati wengi wakidhani Taye kastaafu lakini kumbe sivyo. Jamaa bado yuko uwanjani akicheza soka. Alistaafu kuchezea timu ya taifa akiwa kacheza mechi 54 pekee huku akifunga magoli 8.
Huyu ndiye Taye Taiwo fullback ya kazi kutoka Nigeria.
Sport STAR TV