16/02/2025
Ujenzi JNHPP Wafikia Asilimia 99, Yaleta Tabasamu kwa Watanzania
Na Mwandishi wetu- Rufiji
Ujenzi wa mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 2,115 za umeme umefikia asilimia 99.80 ya utekelezaji wake kufikia Februari 15, 2025, ukiwa na thamani ya fedha za Kitanzania shilingi trilioni 6.558.
Akieleza kuhusu mradi huu, wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo Februari 16, 2025,uliofanyika Rufiji mkoani Pwani, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamadini, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Bw. Gerson Msigwa amesema ukubwa wa mradi huo unawafanya Watanzania watembee kifua mbele ndani ya Afrika Afrika Mashariki akisema “Hakika Watanzania Tumeweza”.
Akieleza kuhusu hali ya utekelezaji wa mradi kwa ujumla, Bw. Msigwa amebainisha kuwa hadi kufikia Februari 15, 2025 mitambo nane kati ya tisa tayari inazalisha jumla ya Megawati1880, huku mtambo namba moja ukiwa katika hatua za mwisho za usimikaji na unatarajiwa kuanza majaribio mwishoni mwa mwezi Februari 2025.
Ameeleza kuwa sehemu nyingine muhimu katika utekelezaji wa mradi wa JNHPP ni utekelezaji wa mradi wa kusafirisha umeme kutoka JNHPP hadi Chalinze – kV 400, yenye urefu wa km 160 ambao umefikia asilimia 99.5 ikilinganishwa na asilimia 44 mwaka 2021/22.
“Aidha, ujenzi wa kituo cha kupoza Umeme cha Chalinze ambacho ni sehemu ya mradi huo umefikia asilimia 92 ikilinganishwa na asilimia 35.9 mwaka 2021/22. Ukamilishwaji wa miundombinu hii imewezesha umeme kusafirishwa kutoka kituo cha kuzalisha umeme cha JNHPP hadi Chalinze na kuingizwa kwenye Grid ya Taifa,” amesema Msigwa
Kuhusu malipo kwa Mkandarasi Msigwa amesema thamani ya ujenzi wa mradi wa JNHPP ni shilingi trilioni 6,558,579,983,500.28 ambapo hadi kufikia mwezi Februari 2025, mkandarasi alikuwa amelipwa kiasi cha Shilingi trilioni 6,289,992,351,216.53 ambacho ni sawa na asilimia 95.90 ya malipo yote.
Msemaji Mkuu wa Serikali
Samia Suluhu Hassan
Ikulu Mawasiliano