
10/01/2025
Rais mteule wa Marekani Donald Trump anatarajiwa kuhukumiwa leo Ijumaa asubuhi kwa saa za huko katika mahak**a ya New York kwa kughushi rekodi za biashara. Mei mwaka jana alipatikana na hatia kwa makosa 34 yanayohusiana na malipo ya kutunza siri aliyolipwa nyota wa filamu za ngono Stormy Daniels.
Daniels alilipwa dola za kimarekani 130,000, ili anyamaze na asizungumzie kuhusu madai yake kwamba alifanya mapenzi na Trump. Trump amekana kuwa walifanya ngono na mwanamke huyo, na amekanusha makosa yoyote.
Hukumu hiyo inakuja baada ya jana usiku Mahak**a ya Juu kukataa ombi la Rais Mteule Donald Trump la kuchelewesha hukumu ya kesi hiyo. Jaji katika kesi hiyo, Juan Merchan, amedokeza kuwa hatampeleka Trump gerezani, na hatawekwa katika kipindi cha uangalizi wala hatopigwa faini.
Trump hatarajiwi kuhudhuria hukumu hiyo ana kwa ana na kuna uwezekano atahudhuria kupitia video. Trump ndiye rais mteule wa kwanza wa Marekani, au rais, kuhukumiwa kwa uhalifu.