
11/07/2025
Tanzania imechomoza kuwa nchi ya nne barani Afrika kwa uzalishaji wa dhahabu, nyuma ya mataifa yenye historia ndefu ya madini ikiwemo Afrika Kusini, Ghana na Mali, ikichangia asilimia 1.3 ya dhahabu yote duniani.
Takwimu zinaonesha kuwa tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani mwaka 2021, uzalishaji wa dhahabu umepaa kutoka tani 55.6 mwaka 2020/21 hadi kufikia wastani wa tani 60,000 mwaka wa fedha 2024/25, hatua inayoashiria mafanikio makubwa katika sekta ya madini.
Mauzo ya dhahabu pia yamevuka matarajio, yakifikia TZS trilioni 7.27 kwa mwaka 2023 kutokana na uuzaji wa tani 55. Hali hii imechochewa na kuimarika kwa bei ya dhahabu duniani, ambayo kwa mwaka 2024 ilifikia wastani wa dola 2,386 kwa ounce, huku robo ya mwisho ya mwaka ikirekodi hadi dola 2,663 kwa ounce.
Mnamo Januari 2025, sekta ya madini nchini iling’ara kwa kufanikisha biashara ya madini ya jumla ya dola bilioni 4.1, ambapo dola bilioni 3.4 zilihusiana moja kwa moja na dhahabu pekee. Hili linawakilisha zaidi ya asilimia 50 ya mauzo yote ya nje ya bidhaa zisizo za kawaida (non-traditional exports).
Mafanikio haya yametokana na sera thabiti za serikali ya awamu ya sita, ikiwemo ile ya kuwataka wachimbaji wakubwa kutenga asilimia 20 ya uzalishaji kwa ajili ya usindikaji na biashara ndani ya nchi, hatua iliyosaidia kuongeza mapato ya ndani na kukuza uchumi.
Kwa ujumla, mchango wa sekta ya madini kwenye Pato la Taifa (GDP) umekua hadi kufikia asilimia 10.1 mwaka 2025, lengo lililowekwa mapema na serikali likitimia ndani ya muda mfupi.