21/10/2025
Waislam wenye kuishi na baadhi ya maradhi hawatoruhusiwa kuingia nchini Saudi Arabia kwenda kutekeleza ibada ya hijja kwa mwaka 2026.
Daktari dhamana wa afya za mahujaji, Naufal Kassim Mohammed, ameeleza hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika msikiti Jamii Zinjibar uliopo Kiembe Samaki.
Aliyataja maradhi hayo ni pamoja na figo linalohitaji kufanyiwa usafishaji, moyo, mapafu yanayohitaji matumizi ya oksijini, maradhi ya ini na uti wa mgongo unaomzuia mgonjwa kufanya shughuli za kawaida.
Maradhi mengine ni mishipa ya fahamu inayosababisha ulemavu wa viungo, uzee, shida ya akili, ujauzito, maradhi ya miguu yanayosababisha mtu kushindwa kutembea kwa masafa na waliopo kwenye matibabu ya saratani.
Alisema kuwa maelekezo hayo wameyapokea kutoka kwa mamlaka inayosimamia ibada ya Hijja kutoka nchini Saudi Arabia, hatua ambayo inalenga kulinda afya za wenye nia ya kwenda kutekeleza ibada hiyo.
Dk. Naufal alikumbushia kuwa miongozo inayotakiwa kufuatwa kwa kila taasisi zinazosimamia mahujaji ni kuhakikisha wanapima afya za mahujaji watarajiwa wakati wa kujiandikisha.
Miongozo mengine kwa taasisi inayochukua mahujaji wa jinsia ya k**e na kiume inatakiwa kuwa na madaktari angalau wawili, mmoja kutoka kila jinsia.
Soma zaidi: 𝐳𝐚𝐧𝐳𝐢𝐛𝐚𝐫𝐥𝐞𝐨.𝐜𝐨.𝐭𝐳