ASAM MEDIA

ASAM MEDIA Contact information, map and directions, contact form, opening hours, services, ratings, photos, videos and announcements from ASAM MEDIA, Media/News Company, KIJANGWANI, Zanzibar.

18/12/2025

Katika kuhakikisha wamiliki na waendesha vyombo vya moto wanatii sheria zilizowekwa ikiwemo ulipaji wa tozo zinazotakiwa, Mamlaka ya Usafiri na Usalama Barabarani kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi wamefanya operesheni maalum ya kukagua vyombo vya moto vinavyotoa huduma za kusafirisha wananchi katika eneo la Mwanyanya, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Akizungumza kuhusu operesheni hiyo, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri na Usalama Barabarani, Ndg. Haji Ali Zubeir, amesema wamebaini uwepo wa vyombo vingi vinavyotoa huduma hizo vikiwa na madeni pamoja na kutokupasishwa, jambo ambalo ni kosa kisheria.

Aidha, Ndg. Zubeir amewaasa wamiliki wa vyombo vya moto kutii sheria bila ya shuruti kwa kuhakikisha vyombo vyao vinakidhi vigezo vilivyowekwa.

16/12/2025

“Lishe na maisha huanza pale ambapo samaki hupatikana.”
Kauli hii inaeleza kwa uwazi umuhimu wa samaki mkunga katika jamii za pwani na mito ya Tanzania.

Leo, mtazamaji wa ASAM ONLINE TV, nakusimulia simulizi fupi inayomuelezea kiumbe huyu wa majini anayejulikana k**a samaki mkunga.

Samaki mkunga ni samaki mwenye thamani kubwa katika maisha ya jamii. Licha ya kuwa mdogo kwa muonekano, amejaa virutubisho muhimu na ni chanzo kikuu cha protini kwa familia nyingi. Zaidi ya lishe, samaki huyu ni kiashiria cha mshik**ano, ushirikiano na maisha ya kijamii.

Kila kukicha, wanawake na wanaume wa kijiji hukusanyika kwa pamoja wakielekea baharini au mtoni, wakivua samaki mkunga kwa kutumia nyavu na mitambo ya mikono. Wakati wa uvuvi huo, hujengwa furaha, mshik**ano na mawasiliano ya kijamii, hali inayodhihirisha nguvu ya umoja katika kazi za kila siku.

Samaki hawa hupikwa mara moja nyumbani na kuwa sehemu muhimu ya chakula cha familia. Wengine hupakwa chumvi au kuuzwa sokoni, hatua inayochangia kuongeza kipato cha kaya na kuimarisha uchumi wa familia.

Mbali na lishe ya kila siku, samaki mkunga una nafasi ya pekee katika sherehe na tamaduni za kijamii. Katika harusi, sherehe za kuaga wageni au hafla mbalimbali za kijamii, samaki huyu hupikwa kwa heshima kubwa, akiwakilisha ukarimu, mshik**ano na heshima kwa wageni.

Kwa hakika, ingawa samaki mkunga ni mdogo kwa muonekano, thamani yake ni kubwa. Hutoa lishe, huimarisha uchumi wa kaya, na huunganisha jamii katika shughuli za kila siku pamoja na sherehe za kitamaduni.

Kwa kweli kabisa, samaki mkunga si chakula tu — ni ishara hai ya maisha, utamaduni na mshik**ano wa jamii za pwani.

Simulizi hii imelenga kuenzi na kuonesha maisha, tamaduni na urithi wa jamii za pwani kwa wapenda utamaduni wa Tanzania.

16/12/2025

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesisitiza kuwa haitasita kuwachukulia hatua kali za kisheria wamiliki wa magari yanayobeba mchanga, kifusi pamoja na kokoto watakaokiuka taratibu na sheria zilizowekwa.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Mheshimiwa Nadir Abdullatif, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi zake zilizopo Maisara, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Waziri Nadir amesema kuwa ukiukwaji wa taratibu hizo unasababisha athari mbalimbali ikiwemo uharibifu wa miundombinu ya barabara, uchafuzi wa mazingira pamoja na kuhatarisha usalama wa watumiaji wa barabara.

Ameongeza kuwa Serikali imeweka mifumo na miongozo maalum ya uendeshaji wa shughuli za uchimbaji na usafirishaji wa mchanga, kifusi na kokoto, hivyo ni wajibu wa wamiliki wa magari na wadau wa sekta hiyo kuzingatia sheria hizo ili kuepuka hatua za kisheria.

Aidha, Waziri huyo ametoa wito kwa wadau husika kushirikiana na Serikali katika kulinda miundombinu na mazingira kwa maendeleo endelevu ya Zanzibar.

16/12/2025

Mkuu wa Wilaya ya Mjini, Ndg. Mohammed Ali Abdallah, ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, amefanya ziara maalumu ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Serikali inayojengwa katika Wilaya ya Mjini.

Ziara hiyo imefanyika kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Mjini, ikiwa na lengo la kutathmini hatua za utekelezaji wa miradi hiyo na kuhakikisha inakamilika kwa wakati ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa ametembelea miradi mbalimbali ikiwemo Kituo cha Afya Daraja la Pili Sebleni, Kituo cha Afya Mpandae Soko la Mombasa, Hospitali ya Wagonjwa wa Akili Kidongo Chekundu, Kituo cha Mabasi ya Umeme Malindi pamoja na Kiwanja cha Mpira kilichopo pembezoni mwa kituo hicho cha mabasi ya umeme.

Kwa mujibu wa taarifa za utekelezaji, miradi yote iliyotembelewa imefikia asilimia 90 ya utekelezaji, hali inayoashiria kuwa iko katika hatua za mwisho za kukamilika.

Mkuu wa Mkoa amesisitiza umuhimu wa wasimamizi wa miradi kuendelea kusimamia kwa karibu ili miradi hiyo ikamilike kwa ubora unaotakiwa na kuanza kutoa huduma kwa wananchi kwa wakati uliopangwa.

16/12/2025

Katika kuhakikisha barabara zinakuwa salama kwa watumiaji wake, Mamlaka ya Usafiri na Usalama Barabarani kwa kushirikiana na Baraza la Manispaa imefanya operesheni maalum ya kuwaondoa wafanyabiashara waliokuwa pembezoni mwa barabara katika soko la Kinyasini, kwa lengo la kuzuia ajali zisizo za lazima.

Akizungumza kuhusu operesheni hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri na Usalama Barabarani, Ndugu Haji Ali Zubeir, amesema zoezi hilo ni endelevu na amewataka wananchi kuzingatia na kutii sheria pamoja na kanuni zilizowekwa kwa ajili ya usalama wa wote.

16/12/2025

Barabara ni miundombinu muhimu inayounganisha miji na vijiji, na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Dkt. Hussein Ali Mwinyi imeendelea kuboresha na kujenga barabara za kisasa ili ziweze kutumika na wananchi wote kwa ufanisi.

Hata hivyo, licha ya juhudi hizo, bado baadhi ya wananchi wamekuwa wakitumia barabara na maeneo ya watembea kwa miguu kwa shughuli zisizofaa, ikiwemo kufanya biashara katika maeneo yaliyotengwa kupitisha watu na misingi ya maji, hali inayosababisha usumbufu kwa watumiaji.

Kutokana na changamoto hiyo, Mamlaka ya Usafiri na Usalama Barabarani Zanzibar imefanya operesheni maalum ya kukagua Barabara ya Kinyasini, Mkoa wa Kaskazini Unguja. Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Ndg. Haji Ali Zubeir, amewataka wafanyabiashara kuacha kuweka bidhaa barabarani, akibainisha kuwa kitendo hicho ni kinyume cha sheria, kinaathiri miundombinu na kinaongeza hatari ya ajali.

Baadhi ya wananchi na madereva wamepongeza zoezi hilo, wakisema litaimarisha usalama barabarani na kuboresha mazingira ya matumizi ya barabara.

08/12/2025

Siku ya jana, Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) kilikabidhi Tuzo za Msimu wa 5 za Kupinga Udhalilishaji wa Kijinsia kwa mwaka 2025, tukio lililowakutanisha wanaharakati, wanahabari, pamoja na maafisa wa madawati ya jinsia walioko mstari wa mbele kupambana na udhalilishaji—ikiendelea na mwendelezo wa Siku 16 za Kupinga Udhalilishaji wa Kijinsia.

Mgeni rasmi wa hafla hiyo alikuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ambaye alipongeza juhudi kubwa zinazofanywa na asasi za kiraia katika mapambano dhidi ya vitendo vya udhalilishaji.

ASAM Online TV imeibuka miongoni mwa washindi wa tuzo hizo kupitia kipengele cha Mwandishi Bora wa Taarifa za Kupinga Udhalilishaji 2025.

02/12/2025

Wakulima wa bonde la Cheju na Kilombero wametoa malalamiko yao kuhusu changamoto za ukosefu wa umeme, upatikanaji hafifu wa maji, pamoja na kushamiri kwa wadudu aina ya paya wanaoharibu mashamba ya mpunga.

Malalamiko hayo yametolewa mbele ya Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar, Mhe. Suleiman Masoud Makame, wakati wa ziara yake yenye lengo la kufuatilia maendeleo na changamoto za miradi ya kilimo cha umwagiliaji na mifugo katika mikoa ya Kusini na Kaskazini Unguja.

Waziri Suleiman ameahidi kutatua kwa haraka changamoto hizo, huku nyingine zikielekezwa kutafutiwa ufumbuzi wa papo kwa papo. Amehimiza wakulima kuendeleza kilimo chenye tija ili kuongeza uzalishaji na kuisaidia nchi katika sekta ya kilimo.

22/11/2025

Wizara ya Afya Zanzibar imetoa taarifa kufuatia malalamiko ya familia ya mtoto Said Abdallah Khamis, baada ya kudaiwa kukosa huduma stahiki katika Hospitali ya Rufaa ya Lumumba.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za wizara hiyo zilizopo Vuga, Wilaya ya Mjini, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar, Dkt. Mngereza Mzee Miraji, amesema wizara imesikitishwa na tukio hilo na imechukua hatua za haraka kuhakikisha uchunguzi wa kitaaluma unafanyika.

Dkt. Mngereza amesema kufuatia tukio hilo, wahusika wa zamu ya siku hiyo wamesimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi huru na wa kina, utakaobaini ukweli wa kilichotokea na kuwajibisha wale wote watakaopatikana na makosa.

Wizara imetoa pole kwa familia ya mtoto huyo na kusisitiza kuwa itaendelea kuhakikisha huduma za afya nchini zinatolewa kwa weledi, uadilifu na kuzingatia haki za wagonjwa.

22/11/2025

Gari lililobeba kontena limesababisha ajali mbaya katika maeneo ya Amani Round About, Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi, usiku wa tarehe 21 Novemba 2025 majira ya saa 2.

Kwa mujibu wa mashuhuda, chanzo cha ajali hiyo kinadaiwa kuwa ni kufeli kwa breki za gari hilo, na kusababisha kupoteza mwelekeo kabla ya kuparamia vyombo vingine vya usafiri na watembea kwa miguu. Inasadikika kuwa watu kadhaa wamepoteza maisha, ingawa idadi kamili bado haijathibitishwa na mamlaka husika.

Vyombo vya ulinzi na usalama vimewasili eneo la tukio kwa ajili ya kutoa msaada wa dharura, kufanikisha uokozi na kuanza uchunguzi wa kina kuhusu chanzo kamili cha ajali hiyo.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dk. Hussein Ali Mwinyi, amemteua Mkurugenzi wa Mamlaka...
20/11/2025

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dk. Hussein Ali Mwinyi, amemteua Mkurugenzi wa Mamlaka ya Uhifadhi na Uendelezaji Mji Mkongwe, Mhandisi Ali Said Bakari, kuwa Katibu katika Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

19/11/2025

MLANDEGE FC NA MALINDI SC WATAMBIANA KUELEKEA DABI YA MJINI

Address

KIJANGWANI
Zanzibar

Alerts

Be the first to know and let us send you an email when ASAM MEDIA posts news and promotions. Your email address will not be used for any other purpose, and you can unsubscribe at any time.

Share