24/07/2025
TANZANIA YAPONGEZWA AFRIKA KUIDHINISHA MATIMIZI YA MBEGU ASILI KWA USALAMA WA CHAKULA.
M***a Juma, Serengeti Media Centre -Ethiopia.
Serikali ya Tanzania imepongezwa kuwa ni miongoni mwa nchi chache barani Afrika,kupitisha mkakati wa kitaifa wa kuzitambua na kuzilinda mbegu za asili, ili kujihakikishia usalama wa chakula.
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe katika msimu wa mwaka 2024/25, ameidhinisha kusajiliwa matumizi ya mbegu 13 za asili za mazao mbali mbali ili zitumike na wakulima kwa mujibu wa sheria ya mbegu ya Tanzania, sura 308 kifungu cha 12(a) na 13(3).
Katika ufunguzi wa mkutano wa kujadili sera zinazoongoza mifumo ya chakula barani Afrika,Mratibu mkuu Shirika la kimataifa la Muungano wa Uhuru wa Chakula Afrika (AFSA) Dk.Million Belay na aliyekuwa Mwenyekiti wa K**ati ya bunge la Afrika Mashariki(EALA) ya kilimo, Utalii na Maliasili, Francoise Uwumukiza, walisema hatua ambayo imefikiwa na Tanzania na serikali ya Kenya kutambua mbegu za asili inafaa kuingwa na mataifa mengine.
Dk. Belay alisema ili bara la Afrika liwe na usalama wa chakula ni muhimu sana kuendeleza na kuzilinda mbegu za asili badala ya kutegemea mbegu za mazao mbali mbali kutoka nje ya Afrika.
"Bara la Afrika kwa miaka iliyopita lilikuwa ndio wazalishaji wakubwa wa chakula, kutokana na uwepo maarifa ya asili katika kilimo, lakini sasa limegeuka bara la kutegemea kila kitu kutoka nje ya Afrika zikiwepo mbegu za mazao"alisema
Dk.Belay alisema kutokana na mabadiliko ya tabia nchi yanayoendelea duniani na kulinda afya ya udongo, usalama wa chakula na baianuawai bara la Afrika linapaswa kuzilinda na kuzitumia mbegu zake za asili na kuendeleza kilimo Ikolojia.
Kwa upande wake, Mbunge wa EALA, Uwumukiza alisema Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, inatambua umuhimu wa mbegu za asili na inaunga mkono jitihada zilizofikiwa na serikali za Tanzania na Kenya kuanza kuzitambua mbegu hizo kwa kuzisajili.
Alisema utambuzi wa mbegu hizo ni utekelezaji wa miongozi ya Umoja wa nchi huru za Afrika, katika kulinda usalama wa chakula barani Afrika.
"EALA tutaendelea kutunga sera na sheria za kulinda mbegu za asili lakini tunaomba nchi nyingine barani Afrika nazo kuzitambua mbegu za asili na kuanza kuzilinda"alisema
Waziri wa Mipango na Maendeleo wa Ethiopia, Fitsum Assefa Adela alisema suala la usalama wa chakula barani Afrika ni muhimu kuendelea kujadiliwa na kuwekewa mikakati ya kudumu.
"Serikali ya Ethiopia inatambua umuhimu wa uwepo wa usalama wa chakula kwa ajili ya kulinda afya na watumiaji wa chakula lakini kujikinga pia na njaa"alisema
Kwa upande wake, Meneja miradi wa shirika la SIDA Afrika,Ayele Kebede Gebreyes, alisema shirika hilo kwa kushirikiana na mataifa mengine yataendelea kusaidia miradi ya kuhakikisha bara la Afrika linakuwa na usalama wa chakula.
Wakizungumzia hatua ya serikali ya Tanzania kuidhinisha matumizi ya mbegu za asili, Afisa miradi wa Shirikisho la wakulima Tanzania(SHIWAKUTA) ambaye pia ni Afisa miradi wa vikundi vya wakulima Arusha(MVIWAARUSHA) Damian James Sulumo alisema wanaishukuru serikali kuzitambua mbegu za asili.
"haikuwa kazi ndogo serikali kufikia uamuzi huu, tuliunda kikosi kazi cha masuala ya mbegu na kujadiliana na serikali na k**ati ya bunge la kilimo hadi kufikia makubaliano ambayo ni faraja kubwa kwetu"alisema
Sulumo alisema wizara ya kilimo, pia katika bajeti ya mwaka 2005/26 ilizungumzia umuhimu wa mbegu za asili na kuahidi kuendeleza tafiti zaidi ikiwepo ujenzi wa kituo maalum cha utafiti mkoani Arusha.
Afisa Ushawishi na utetezi wa SHIWAKUTA, Thomas Laizer alisema haiwezekani kuwa na mapinduzi ya kilimo kwa kutegemea mbegu kutoka nje ya Afrika na kuzitaja mbegu za asili zilizoidhinishwa Tanzania ni aina nne(4) ya mbegu za mahindi, Mpunga mbegu aina 4,mbegu za maharage aina mbili(2) na Papai aina tatu(3).
"Tanzania tumejaliwa kuwa na mbegu nyingi na nzuri za asili ambazo tunaamini zikitumika vizuri tutaongeza uzalishaji wa chakula lakini pia utakuwepo usalama wa chakula wakati wote na kuacha kutegemea mbegu kutoka nje ya nchi wakati wote" alisema.
Mkutano huo wa Usalama wa chakula unaendelea katika jiji la Addis Ababa ambapo nchi 23 barani Afrika zinashiriki, wakiwepo watafiti wa mazao, wataalam wa kilimo Ikolojia( Hai) wabunge, viongozi wa serikali, asasi za kiraia na waandishi wa habari.