
04/08/2025
AHMED ALLY AWATULIZA MASHABIKI KUHUSU MPANZU: "YUKO WAPI?"
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba SC, Ahmed Ally, ameibuka na kuwashangaa baadhi ya wachambuzi na wanahabari wanaoeneza taarifa zisizo na uhakika kuhusu mchezaji wao Elie Mpanzu.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Ahmed amesema amebaki kushangazwa na kauli zinazokinzana kutoka kwa watu wale wale waliodai awali kuwa Mpanzu hayuko Misri, lakini sasa wamesema ameonekana nchini humo.
“Kinachonishangaza ni kwamba watu waliokuwa wakisema Mpanzu hayupo Misri, ni hao hao leo wanasema amefika Misri,” ameandika Ahmed, huku akiwataka wenye taarifa za uhakika wamsaidie kwa kumwelekeza mchezaji huyo kwani wao hawajamuona.
Ameongeza kuwa si vema kueneza taharuki kwa mashabiki, bali watu waendelee kuwa na amani huku wakisubiri taarifa rasmi kutoka kwa klabu.
Katika siku za karibuni, kumekuwepo na ongezeko la taarifa na tetesi mbalimbali kuhusu usajili wa wachezaji baina ya vigogo wa soka nchini — Simba SC na Yanga SC — hali inayowaweka mashabiki wa pande zote za Kariakoo katika hali ya taharuki.
SWALI KWA MASHABIKI:
JE, UNADHANI ELIE MPANZU ATABAKIA SIMBA AU ATAELEKEA YANGA? NA JE, NAFASI YAKE YA KUNG'AA NI KUBWA ZAIDI AKIWA SIMBA AU YANGA?
TUJADILIANE.